KNEC KCSE Kiswahili Paper 2 Question Paper / 2015 KCSE Kirinyaga West
2015 KCSE Kirinyaga West
Kiswahili Paper 2
1. UFAHAMU (Alama 15)
Soma taarifa ifuatayo kisha ujibu maswali yanayofuatia
Shule yangu ya upili
Majio yangu katika shule hii ya upili hayakutokea kwa bahati nasibu bali kwa mipango kabambe niliyoianza tangu nikiwa shule ya vichekechea. Nikiwa sitetereki hata kwa wazazi wangu waliponisihi nijiunge na shule nyingine za karibu nikawa sisikii la mwadhini wala la mteka maji msikitini. Nikawa na ragba ya mkanja nikingoja siku ya kujiunga na shule yenyewe. Kweli majuto ni mjukuu na huja kinyume.
Nilizaliwa katika aila yenye nafasi iliyotopea na kubobea katika ukwasi uliodhihirika kutokana na mitaa tulikoselelea kwa muda kabla ya baba kuaamua kununua nyumba yake mwenyewe huko upande wa Karen hivyo tukagura kutoka Runda. Wakati wa likizo tukawa tunaruka hadi pwani ambako mama yangu alikuwa amemiliki jumba lililokuwa katika ufuo wa bahari lililojengwa katika kipande kisichopungua ekari tatu alilotunukiwa wakati wa nikahi yao na wakwe wa baba yangu.
Wavyele wangu wakawa wanaendesha magari meusi ya kifahari ingawa sikuwahi kumwona mama akichangamka kuendesha magari yake ya maana, kila macheo ya siku za kazi gari lililoendeshwa na dereva ambaye alimstahi mama hadi akawa anamfungulia mlango wa gari na kuufunga baada ya mama kujitoma katika tumbo la gari lilimjia na kumrejesha kwa wakati. Nikajiunga na shule ya msingi ya kibinafsi ambako nilishughulikiwa kama kikembe. Wengi wa wale tuliosoma nao walikuwa wa tabaka langu na walikuwa wametoka katika kila sehemu nchini Kenya.
Hayawi hayawi huwa na siku ya kuripoti ikafika. Alfajiri, dereva mmoja akatumwa kwenda hadi Kisumu ili atulaki na kutusafirisha kutoka uwanja wa ndege hadi shule ya upili ambayo ilikuwa yangu ya rohoni. Nasi tukaelekea hadi uwanja wa ndege ili turuke hadi Kisumu. Safari yetu kutoka kitongoji cha kifahari hadi Airport ilikuwa njema, safari yetu tulipoabiri ndege ilikuwa bila bughudha, safari yetu kutoka Kisumu mjini haikuwa na kasoro na tulienda kulingana na mpango. Safari yetu ilikuwa mufti hadi tulipofika katika lango la shule ya kitaifa!
Tulipotia ozi tu!!….jamani……jamani nikafa moyo. Labda mama aliweza kubaini mabadiliko ya hisia zangu, nilitamauka, nikawa mchege na kusema kweli niliyoyaona sikuamini. Mvua iliyokuwa imepasua hapo awali ilikuwa imeacha vitua vya maji kwenye vijia vya kutembea vilivyochakaa na kubomoka bila yeyote kujali kuvikarabati. Majengo yalikuwa makongwe yaliyojengwa miaka mia moja iliyopita na yalistahili kuitwa makafadhi badala ya pahali pa kumkaribishia mwanafunzi aliyepita kwa alama mia nne na thelathini na tano.
Asiye na wake ana Mungu, nikapiga moyo konde lazima nisajiliwe katika shule ya ndoto langu. Ningewezaje kughairi wazo langu baada ya siku hizo zote za maandalizi tena mbele ya wanuna walioniona kama kielelezo chao tangu walipozaliwa. Nikasajiliwa!
Sikujua, hakika sikujua, sikujua shule ya upili ya kitaifa yaweza kuwa hivi. Kweli mwanafunzi aweza kukosa viatu na hata kushindwa kununua rangi ya kupaka viatu hivyo iwapo amenunuliwa na wahisani? Nilimlaumu ninamaana hakunieleza kuwa mtu anaweza kula chakula ambacho mbwa wetu hawezi hata kukiangalia. Nilipoingia katika ukumbi wa chakula nilihisi kitefutefu nusura nichafukwe na moyo, makapi ya mboga na uchafu usioelezeka ulinikumba, kisha nikapewa kisahani cha plastiki na kupakuliwa kipande cha ugali ambacho bado kilikuwa na unga na kuachiwa hiari ya kukila au kukitupa. Wenzangu wakawa wanakirambatia chakula kwa kasi huku mmoja wao alipoona jinsi nilivyokiangalia changu akanihisi nimpe chote na kukimaliza fyu. Wote walikuwa na furaha kemkem na kuajabia utukufu wa shule iliyotukuka ya kitaifa ila mimi.
Baada ya mlo ‘rojo rojo’, tukaelekea darasani nilikopigwa na mghuma mkubwa. Tulikuwa wanafunzi hamsini na watano katika darasa moja tu! Mwalimu mmoja akaja na kutukaribisha shuleni kisha akatuarifu kuwa atakuwa mwalimu wa darasa letu. Nilipomsikia akinena nusura niishiwe na stahamala, kimombo chake kilinishangaza, hasa matamshi yake yalipungukiwa na kudhirisha athari za lugha ya asili. Nilihisi kana kwamba ningemrekebisha lakini sikudhubutu.
Tukafululiza hadi bweni na nikajilaza kitandani chembamba huku mwingine nisiyemjua lakini asiyejua kuwa kuna nguo maalum za kulala akalala uchi katika ghorofa ya juu ya kitanda chetu. Mgeni njoo mwenyeji apone maana baada ya muda wadudu ambao sikuwahi kuwaona aushini mwangu wakanza kunishambulia. Nikaamka baada ya kumnasa mmoja wa wadudu hawa na kuuliza mmoja wa wenzangu ni wepi wadudu hawa na kwa kutojali hata kidogo, akanieleza kuwa hawana neno bali ni kunguni tu, sikujua na kwa kweli mama hakuniambia kuwa kuna wadudu wanaotafuna mtu na hunuka fye! Sikulala kwa hofu huku wenzangu wakiforota kwa njia ya kunighasi. Sikuwahi kudhani kuwa watu wengi wanaweza kulala chumba kimoja huku changu kikiwa na hamamu na vifaa vyote muhimu kikibaki bila mtu!
Tulisomeshwa na walimu wasiojali kana kwamba tunaelewa au la. Hawakushughulika iwapo tulifanya kazi za ziada au la, ndio, hakujali chochote. Kilichonishangaza ni kuwa wanafunzi waliojiunga nasi kutoka shule za umma wenye alama duni waliwapenda na kuelewa haraka walichosomeshwa na hawakujali matamshi yao, labda hawakuyatambua.
Hatimaye tukafanya mtihani wa mwisho wa muhula wa kwanza. Nilishangaa ghaya iliponibainikia kuwa aliyetuongoza alikuwa ghulamu mmoja mshamba niliyempuuza tu mvulana kutoka kijijini ambacho singetambua katika ramani ya nchi ambaye hata vitu vya kimsingi vilimpiga chenga. Nikafanya uchunguzi nikatambua mwenzangu alikuwa na alama mia mbili hamsini na tatu akitoka katika darasa la nane, nilifanikiwa kuwa nambari mia mbili hamsini na tatu kwa jumla ya wanafunzi mia tatu!
Tulipofunga kwa likizo ya Pasaka nikaamua kuchukua hatua nyingine sitawahi kuhama kutoka shule hii ya upili wala kuwa zaidi ya nambari kumi!
Maswali
a) Thibitisha kauli kuwa msimulizi ana msimamo dhabiti (alama 2)
b) Tofautisha jinsi mwandishi alivyofunzwa katika shule ya kibinafsi na shule ya upili. (alama 3)
c) Taja mambo matatu yanayotuonyesha kuwa msimulizi alilelewa katika aila ya kikabaila kulingana na aya ya pili.(alama 3)
d) Andika masuala matatu yaliyomshangaza katika shule ya upili (alama 3)
e) Andika tamathali mbili zilizotumika katika kifungu. (alama 2)
f) Eleza maana ya msamiati huu kama ulivyotumika katika kifungu. (alama 3)
i) alimstahi
ii) kughairi
iii) kunighasi
15 marks
2.UFUPISHO (Alama 15)
Soma habari ifuatayo kisha ujibu swali
Tulipigwa na butwaa kwa kupokea habari kuhusu mauaji ya wasafiri 28 waliouwawa kikatili huko Mandera na kabla kuwasidikiza makaburini wengine waliokuwa 40 wakijitafutia riziki katika chimbo la mawe kuko huko, wakaangamizwa. Tunapinga na kulaani vikali visa vya ugaidi vinavyoendelezwa kutetemesha usalama wa wananchi. Hivi ni vitendo vya kinyama vinavyotekelezwa na watu waliokosa ubinadamu na utu kabisa. Inakera mno kwa vitendo vya kigaidi. Inagadhabisha kuona Wakenya wasio na makosa wakiteswa na kuuwawa kinyama bila huruma na watu wasio na utu. Hatuogopi wala hatuna fedheha kuamba magaidi hawa wamelaaniwa na siku zao zimehesabiwa hapa duniani, damu ya mwananchi asiye na makosa katu watailipia. Napinga vikali pale magaidi hawa wanapohusisha vitendo hivi kuwa vita vya kidini. Vita hivi si vya kidini kwani hakuna dini yoyote iliyo na imani ya kumwua kinyama binadamu asiye na makosa.
Kando na tishio la ugaidi, Wakenya pia wanakabiliwa na hatari za ujambazi, mauaji, unajisi, ubakaji na maovu mengine. Iwapo mbunge anayelindwa na askari wawili atawauwa, je wananchi wa kawaida watakosa kumuua?
Katika juhudi za kudumisha usalama, polisi wana jukumu la kutumia kila mbinu kuhakikisha kuwa haki ya kikatiba ya Wakenya kuhusu kulindwa kwa maisha na mali yao imedumishwa. Polisi nao wanashambuliwa huko Kapendo na kumiminiwa marisasi wasiweze kujikinga tukabaki kuwazika licha ya umri wao mdogo ili kukabiliana na tatizo hili, polisi wakaamua kusaka wahalifu. Lakini cha kusikitisha kuwa mbinu ambazo polisi wamekuwa wakitumia hasa hii ya kufanya misako inayoishia kuwanasa mamia ya raia wasio na habari kinachoendelea, inawaongezea Wakenya mateso. Hali hii inawaacha Wakenya kwenye hatari ya kunaswa na majambazi ama polisi.
Matumizi ya mbinu hii ya misako imeishia kunasa raia wengi wasio na makosa. Wanaponaswa, hurundikwa kwenye seli usiku mzima ama siku kadha na hata kama wanaachiliwa huwa tayari wameteseka. Huu ni ukiukaji wa haki za raia. Kadhalika, mbinu hii yaonekana kama hila ya polisi kutaka kuonyesha wanafanya kazi lakini sio mwafaka kwani wanapokuwa wakiwanasa raia mijini na mitaani, magaidi na majambazi wanaendelea na shughuli zao.
Badala ya kusaka wakora kwa kubahatisha kwenye umati, polisi wanapaswa kubuni njia ambazo zitawapa mwelekeo mwafaka zaidi kuhusu wahalifu ili waweze kuwafuatilia. Ushirikiano baina yao na majajusi uwepo.
Hii itawezesha polisi kupata habari muhimu kuhusu vitisho vya uhalifu. Maafisa wa usalama pia wanaweza kupata habari muhimu kutoka kwa raia. Ni ajabu kuwa sisi tunaelekeza kidole cha lawama kwa serikali ilhali wahalifu hawa tunaishi nao katika mitaa tunakoishi, viongozi wapinzani wasipinge mikakati yoyote ya serikali kama vile mpango wa nyumba kumi kisa na maana si wazo lao. Iwapo hawapendezwi na mpango kama huo waibuke na mbinu badala tuzijaribu. Suala la ‘serikali ingilie kati’ hata bwana mlevi anapochapwa na mkewe lisukumwe katika kaburi la sahau.
Maswali
a) Ni nini maoni ya mwandishi kuhusu suala la ugaidi?
Tumia maneno 80 (alama 7, 1 utiririko)
Matayarisho
Nakala safi
b) Kwa kutumia maneno yasiyozidi 50, fupisha aya mbili za mwisho (alama 6, 1 utiririko)
Matayarisho
nakala safi
15 marks
3. MATUMIZI YA LUGHA (Alama 40)
Jibu maswali yafuatayo.
Badilisha vitenzi hivi viwe katika hali ya kuamuru
1) kuleta …………………………………………………………………………………………………….
2) kuja ………………………………………………………………………………………………………
2 marks
Tumia kiungo ‘na’ katika sentensi kuonyesha:
1) Ufupisho wa nafsi ya kwanza umoja fulani
2) kihusishi kuonyesha aliyetenda jambo fulani
2 marks
Ainisha vishazi katika sentensi ifuatayo
1) Mwalimu amesema ya kwamba watoto wengi wamekuwa wahuni.
2) Ikiwa nitamwona mama sokoni, nitamweleza kila kitu
2 marks
Ainisha viungo vya kisarufi katika sentensi hii
Alani
3 marks
Tumia kitenzi ‘cha’ katika kauli ya kutendesha katika sentensi
2 marks
Tumia kiambishi ngali katika sentesi kuonyesha hali ya kuendelea.
2 marks
Tofautisha kwa kueleza maana ya istilahi hizi:
ghuna
si ghuna
2 marks
Changanua sentensi kwa njia ya matawi
Yeye na mama yule si watu wazuri sana
4 marks
Eleza sifa bainifu za sauti zifuatazo
i) /I/
ii) /ch/
4 marks
Tumia kielezi cha namna kiigizi katika sentensi
2 marks
Andika sentensi hii upya katika usemi halisi
Mwanafunzi alimsihi mwalimu asimwadhibu wakati huo
2 marks
Onyesha chagizo katika sentensi hii
Mtoto alikula kwa utaratibu jana jioni
2 marks
Tambua na uainishe shamirisho katika sentensi hii
Hamu amemwandikia mwalimu riwaya kwa kalamu
3 marks
Unda vitenzi kutoka kwa maneno haya kisha uyatumie katika sentensi yakiwa katika hali hiyo ya kitenzi
i) Marashi
ii) bora
3 marks
Tofautisha kati ya vivumishi hivi kwa kueleza maana ya kila kimojawapo
i) -ingine
ii) -ingineo
2 marks
Sahihisha makosa katika sentensi hii
Mtoto mgani mwenye kupiga kelele darasani
2 marks
Tumia maneno haya katika sentensi ili kuyatofautisha
shoka
choka
shoga
2 marks
4.ISIMU JAMII (Alama 10)
Jibu swali.
Nani kuku…..? Sosi poa leo …… Mate ndo! ndo! ndo!. Ukimanga hii hutaona daktari kwa miaka kumi……
Ng’ombe je? nani? ……nani!… Ni wewe……. poa basi naja…………
a) Ni sajili gani inayorejelewa hapo juu? (alama 2)
b) Andika sifa za sajili hii ukitoa mifano ndani na nje ya muktadha huu (alama 8)
10 marks