TETEMEKO LA ARDHITAARIFA KWA WAANDISHI WA HABARI NA WANANCHI JUU YA TETEMEKO

LA ARDHI LILILOTOKEA NCHINI

1. UTANGULIZI

Tunatanguliza shukrani za dhati kwa kuweza kuhudhuria katika mkutano huu. Lengo kuu la mkutano huu nikutoa taarifa kwa umma kuhusu namna Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam inavyoshiriki na kushirikiana na watanzania wengine nchini katika kujenga mshikamano wa kitaifa wa kukabiliana na janga la asili liloikumba nchini yetu. Mnamo tarehe 10 Septemba 2016, majira ya saa 9 na dakika 27 mchana, kulitokea tetemeko la ardhi mkoni Kagera lililosambaa katika maeneo mbalimbali ya Kanda ya Ziwa na kusababisha maafa makubwa vikiwemo vifo vya watanzania wenzetu, uharibifu wa makazi ya wananchi na miundombinu ya barabara na majengo ya taasisi zinazotoa huduma za kijamii na kiuchumi. Tunatumia fursa hii kuwapongeza na kuwashukuru kwa dhati wananchi, watumishi wa serikali na vyombo vya ulinzi na usalama, wanahabari, viongozi wa kisiasa na jumuiya ya kimataifa kwa kujitolea kwa hali na mali kukabiliana na janga hili. Tunawaomba muendelee na moyo huo wa mshikamano hadi hapo hali itakapotengamaa na wananchi kuendelea na shughuli zao kama kawaida.

Aidha, tunawapa pole wafiwa wote pamoja na majeruhi. Tunawaombea kwa mola majeruhu wote waweze kupona haraka. Vile vile, tunamwomba mola aziweke roho za marehemu wote mahala pema peponi. Tunawapongeza pia wananchi walioko kwenye maeneo yaliyoathirika na tukio la tetemeko la ardhi kwa kuonyesha moyo wa subira, ustahimilivu na mshikamano katika kipindi hiki kigumu.

Jumuiya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam itaendelea kuchangia katika juhudi za wananchi na serikali za kukabiliana na majanga ya asili nchini. Katika tukio la tetemeko la ardhi la mkoani Kagera, Jumuiya yetu itaendelea kutoa mchango wake njia kuu mbili. Mosi, kutoa elimu na taarifa sahihi kwa umma kuhusu matetemeko ya ardhi. Elimu na taarifa sahihi ni moja ya nyenzo muhimu sana za kukabiliana na majanga ya asili. Tutaendelea kufanya hivyo kwa njia za kutoa mafunzo ya muda mfupi na mrefu na pia kwa kufanya utafiti. Pili, tutahamasisha wanajumuiya wote wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na watanzania wote kwa ujumla kuendelea kujenga mshikamano wa kitaifa wakati wa raha na shida. Kama ilivyo kwa Elimu, mshikamano wa kitaifa ni nyenzo muhimu sana ya kukabiliana na majanga ya asili.

Kwa kipindi cha mwezi mmoja, kuanzia leo tarehe 15 Septemba hadi tarehe 15 Octoba 2016, tutatoa elimu na taarifa kwa umma huhusu matetemeko ya ardhi kwa njia ya vyombo vya habari. Aidha, tutahamasishana na kuwahamasisha watanzania wenzetu ili waendelee kuchangia kwa namna mbalimbali katika kukabiliana na atahari za janga hili. Tunawaomba wanajumuiya kuwasilisha michango yao ya kifedha kupitia akauniti hii ya benki: Jina la Acount: University of Dar es Salaam Self Insurance; Namba ya Akaunti: 040103001175; Jina la Benki: NBC Tawi la Chuo Kikuu cha Dar es

Salaam.

2.ELIMU NA TAARIFA FUPI KUHUSU TETEMEKO LA ARDHI LILOTOKEA KAGERA

Kama tulivyoeleza, tarehe 10/09/2016 saa 9 na dakika 27 mchana kulitokea tetemeko la ardhi mkoani Kagera.

Kiini (focus) cha tetemeko hilo ni kwenye makutano ya latitudo 10 06’ na longitudo 310 55’ eneo ambalo ni kilomita 22 kaskazini mashariki mwa kijiji cha Nsunga na kilomita 42 kaskazini magharibi mwa mji wa Bukoba. Kiini (focus) hicho kilikuwa kilomita 40 chini ya ardhi kwenye eneo hilo. Kitovu (Epicentre) cha tetemeko hilo katika ardhi ya Tanzania ni kijiji cha Rubafu kilichoko katika Wilaya ya Bukoba Vijijini mkoani Kagera.

Nguvu za mtetemo wa ardhi wa tetemeko hilo ni kipimo cha 5.9 kwa kutumia skeli ya “Richter” ukubwa ambao ni wa juu kiasi cha kuleta madhara makubwa juu ya uso wa dunia hasa katika maeneo yalio karibu na kiini cha tetemeko. Kutokana na ukubwa huu maeneo mengi ya mkoa wa Kagera ikijumuisha mji wa Bukoba yamepatwa na madhara makubwa sana ikiwa ni pamoja na nyumba nyingi kupasuka, watu wengi kujeruhiwa kwa kuangukiwa na vifusi na kuta za nyumba. Imethibitika kwamba watu 17 wamepoteza maisha yao.

2.1 Namna Tetemeko la Ardhi Lilivyotokea

Kitovu (focus) cha tetemeko lililotokea Kagera kiko chini sana ya ardhi (km 40), hivyo tetemeko hilo limesababisha miamba mikubwa sana kupasuka kwa ghafla na kutokea kwa misuguano ya vipande vikubwa vya miamba ambavyo viligandamizwa zaidi ya kikomo chake cha mwitikio wa mgandamizo (stress beyond elastic limit). Mipasuko hiyo ni mithili ya ile inayoonekana kwenye bonde la ufa. Tetemeko la ardhi tunaloliongelea limetokea karibu na mkondo wa magharibi wa bonde la ufa la Afrika Mashariki ambapo ni sehemu ambayo matetemeko ya ardhi yanatarajiwa kujitokeza kutokana na uhalisia wa kijiolojia na kijiografia wa sehemu hiyo. Kwa hiyo, matetemeko ya ardhi yanatarijiwa kutokea katika nchi za Afrika Mashariki.

2.2 Jinsi ya Kupima Matetemeko ya Ardhi

Kwa hivi sasa, teknolojia na elimu ya sayansi havina uwezo wa haraka wa kutabiri kwa usahihi kwamba tetemeko la ardhi litatokea. Vifaa vilivyopo vinaweza kupima ukubwa na tabia za matetemeko ya ardhi baada ya kutokea katika eneo husika. Kuna aina tatu ya matetemeko ambayo ni: Tetemeko kuu (main shock) matetemeko madogomadogo kabla ya tetemeko kuu (foreshock) na matetemeko madogomadogo baada ya tetemeko kuu (aftershock). Matetemeko madogomadogo (foreshock) hutokea kabla ya tetemeko kuu (mainshock) ambayo mtu anaweza kusema yangeweza kutumika kujua tetemeko kuu litatokea muda gani. Lakini yote haya yaani (foreshock- mainshock-aftershock) yanapishana katika muda mfupi sana na usiotabirika.

Ukilinganisha na uitikiaji wa kibinadamu (human response) siyo rahisi kutoa tahadhari yoyote kwa muda mfupi ambao tetemeko kuu huwa linatokea.

2.3Mambo Muhimu ya Kuzingatia ili Kupunguza Ukubwa Madhara Kabla ya tukio:

(a)Elimu ya tahadhari inapaswa itolewe kwa wakazi wa maeneo yanayotarajiwa kukumbwa na matetemeko ili kila mkazi aelewe nini cha kufanya linapotokea tetemeko la ardhi ikiwa ni pamoja na kupata mafunzo ya kuwaweka watu katika hali ambayo itasaidia kupunguza madhara ambayo hujitokeza kutokana na matetemeko ya ardhi.

(b)Kufanya mazoezi ya kuchukua tahadhari hizo mara kwa mara ili kujizoesha kwani mara nyingi wakati wa matukio ya majanga ya asili kama hayo watu huchelewa kuchukua uamuzi wa haraka kujinusuru kwani hubabaika na hata kupigwa na butwaa. Hivyo, mazoezi ya mara kwa mara ya jinsi ya kuchukua tahadhari humfanya mtu kufanya uamuzi wa haraka pindi tukio linapotokea.

(c)Wananchi pia wanashauriwa kujenga nyumba zinazoweza kuhimili matetemeko ya ardhi. Ushauri wa kitaalamu unatakiwa kutolewa ili wananchi waweze kujua aina ya majengo yanayofaa kujengwa katika eneo husika ukilinganisha na ardhi ya mahali hapo. Ni muhimu kuepuka ujenzi wa nyumba katika miinuko mikali yenye kuambatana na mawe/ miamba (suspended boulders) na pia kuepuka ujenzi wa makazi katika maeneo tete yenye mipasuko ya miamba na yenye uwezekano mkubwa wa kutokea matetemeko.

Wakati wa tukio:

(a)Wakati wa tukio la tetemeko la ardhi wananchi wanashauriwa kukaa mahali salama kama vile sehemu ya wazi isiyo na majengo marefu, miti mirefu na miinuko mikali ya ardhi.Kiufupi watu wanashauriwa kukaa nje ya nyumba zao katika sehemu za wazi.

(b)Endapo tetemeko litakukuta ukiwa ndani ya nyumba unashauriwa ukae chini ya uvungu wa meza imara au kitanda, ama kusimama kwenye makutano ya kuta na pia ukae mbali na madirisha na makabati ya vitabu, vyombo au fanicha ili kuepuka kuangukiwa na vitu hivyo.

(c)Jiandae kwa matetemo yatakayofuata (aftershock) baada ya tetemo kuu. Tetemeko kuu huwa mara nyingi linafuatiwa na matetemo mengi madogo madogo kwa kipindi cha hadi siku tano. Matetemeko haya yanayofuata huwa yanazidiana kwa kiwango cha ukubwa kwenye kipimo cha Richter scale ambayo kwa kutegemeana na tetemeko kuu nayo yanaweza kuwa makubwa. Tetemeko la ukubwa wa 5.9 linaweza kufuatiwa na lenye ukubwa wa 4.4 au 4.5 (around four point something). Haya matetemeko yanayofuata (aftershock) yanasababisha kuanguka au kubomoka kwa nyumba ambazo zimewekwa nyufa kubwa na tetemeko kuu. Hivyo basi, kwa sababu hiyo watu wanashauriwa wasikae kwenye nyumba zenye nyufa kubwa baada ya tetemeko kuu mpaka watakapopata maelekezo kutoka kwa wataalamu husika.

(d)Baada ya matetemo kumalizika endapo itakulazimu kuondoka mahali ulipo ukiwa katika jengo refu unashauriwa kutumia ngazi badala ya lifti.

4. Hitimisho

Bila shaka, kama taifa, tumeweza kujifunza mambo kadhaa juu ya namna ya kukabiliana na majanga ya asili hasa baada ya tukio hili. Tumejifunza kwamba:

Elimu na taarifa sahihi ni nyenzo madhubuti ya kukabiliana na majanga ya asili. Itabidi taasisi za elimu ya juu na vyombo vya habari vijengewe uwezo wa kifedha na kitaaluma ili kutimiza majukumu yake wakati wa kukabiliana na majanga ya asili. Uwekezaji wa aina hii unatakiwa kuwa endelevu. Jumuiya ya Afrika Mashariki inapashwa kuelekeza nguvu zake katika eneo hili kwani, kijiografia na kijiolojia, karibu nchi zote wananchama ziko katika hatari ya kukumbwa na majanga ya asili

Pindi linapotokea tukio la janga, inabidi nguvu za kukabiliana na maafa zielekezwe kwenye maeneo yaliyoathirika zaidi. Katika tukio hili maeneo yaliyoathirika sana ni vijiji hasa vya wilaya za Bukoba Vijijini, Manispaa ya Bukoba na Misenye. Maeneo ya vijijini, mbako ndiko maafa makubwa yametokea misaada haijapelekwa kwa kiwango cha kuridhisha. Misaada mingi ielekezwe huko. Kipaumbele cha kwanza kiwe ni kutoa misaada ya binadamu hasa chakula, maji safi na salama, makazi ya muda na madawa. Hii ni muhimu ili kuepusha maafa zaidi na hasa kutoe kwa magonjwa ya kuambukizwa

Mshikamano wa kitaifa ni nyenzo madhubuti ya kukabiliana na majanga ya asili. Tunapashwa kujifunza namna Mshikamano wa kitaifa unavyotumiwa na nchi ambazo hukumbwa na majanga ya asili mara kwa mara. Tunaweza kujifunza mengi kutoka nchi za Japan na China. Hata tukio la tetemeko la ardhi lilivyotokea hivi katibuni nchini Italia linaweza kuwa funzo kwetu. Ingawa nchi ya Italia ilipokea misaada kutoka nje, mshikamano wa wananchi wakati wa janga hilo ulijidhihirisha.

Taarifa hii imeandaliwa na viongozi wa Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaa (UDASA), Jumuiya ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DARUSO), Jumuiya ya Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Convocation of UDSM); na Matawi ya Vyama vya Wafanyakazi vya THTU na RAAWU.

Sponsored Links

Leave a Comment