KNEC KCSE Kiswahili Paper 3 – 2014 Nakuru District Mock
2014 Nakuru District Mock
Kiswahili Paper 3
SEHEMU A (Alama 20)
LAZIMA. Soma shairi lifuatalo kisha ujibu maswali yafuatayo.
IMANI YA MWANA
MWANA Kwani mamangu u ng’ombe, au u punda wa dobi?
Nakuuliza usambe, nayavunja madhehebi
Nalia chozi kikombe, uchungu wanisibabi
Hebu nambie
Kweli jaza ya kiumbe, ni madhila na mapigo?
MAMA Nong’ona mwana nong’ona, sitafute angamiyo
Sinipe kuja sonona, kwa uchungu na kiliyo
Babayo mkali sana, kubwa pigo la babayo
Kwani kelele kunena, huyataki maishayo?
Hilo nakwambia
MWANA Sitasakamwa kauli, nikaumiza umiyo
Nikabeba idhilali, nikautweza na moyo
Siuvuwati ukweli, hazidisha gugumiyo
Baba hafanyi halali, nawe huachi vumiliyo
Hebu nambie
Kweli jaza ya kiumbe, ni madhila na mapigo?
Nambie ipi sababu, ya pweke kwenda kondeni
Nini yako matulubu, kulima hadi jioni?
Na jembe ukidhurubu, ukilitua guguni
Yu wapi wako muhibu, Baba kwani simuoni?
Hebu nambie
Kweli jaza ya kiumbe, ni madhila na mapigo?
Baba kwani simuoni, kuelekea shambani?
Kutwa akaa nyumbani, na gumzo mitaani
Hajali hakuthamini, wala haoni huzuni
Mwisho wa hay a ni nini, ewe mwana wa imani?
Hebu nambie
Kweli jaza ya kiumbe, ni madhila na mapigo?
Na kule kondeni kwako, ukate kuni kwa shoka
Ufunge mzigo wako, utosini kujitwika_
Kwa haraka uje zako, chakula upate pika
Ukichekwa vituko, baba anakutandika
Hebu nambie
Kweli jaza ya kiumbe, ni madhila na mapigo?
Chakula kilicho ndani, ni jasho lako hakika
Kiishapo u mbioni, wapita kupokapoka
Urudi uje mekoni, uanze kushughulika
Ukikosa kisirani, moto nyumbani wawaka
Hebu nambie
Kweli jaza ya kiumbe, ni madhila na mapigo?
Na nyumbani ufagie. na nguo zake kufuwa
Wadogo uangalie, wapate kunadhifiwa
Baba umuandalie, kwa sahani na makawa
Hapo we we ubakie, umngojee kunawa
Hebu nambie
Kweli jaza ya kiumbe, ni madhila na mapigo?
Na maungo umkande, umsinge kwa madawa
Mambo yasende upande, kila kitu kiwe sawa
Huoni hata ushinde, utumwa umeachiwa
Natamani nikulinde, na hii yako beluwa
Hebu nambie
Kweli jaza ya kiumbe, ni madhila na mapigo?
Wakati umeshafika, yapasa kujikombowa
Ukae ukikumbuka, haki zenu nyote sawa
Mpaka lini ‘tasumbuka, ukiteseka kwa ndowa
Na nyuma unajiweka, kwa hofu waadhibiwa
Hebu nambie
Kweli jaza ya kiumbe, ni madhila na mapigo?
MAMA Wanitonesha kidonda, cha miaka na miaka
Usidhani nayapehda, madhila pia mashaka
Nakerwa na yake inda, na sasa nimeshachoka
Ninaanza kujipinda, kwa mapambano hakika
Hilo nakwambta!
a) Eleza lengo la mtunzi wa shairi hili. (alama 1)
b) Fafanua ujumbe wa shairi hili. (alama 6)
c) Kulingana na shairi hili, ni sifa gani inamfanya mwanamke kuteswa. (alama 1)
d) Hili ni shairi la aina gani. (alama 2)
e) Eleza maana ya vifungu hivi. (alama 3)
(i) Sitasakamwa kauli.
(ii) Moto nyumbani unawaka. (iii) Siuvuwati ukweli.
f) Tambua kwa kutoa mfano jinsi uhuru wa utunzi ulivyotumiwa na mtunzi wa
shairi hili. (alama 2)
g) Andika ubeti wa tisa kwa lugha ya nathari. (alama 5)
20 marks
SEHEMU YA B (Alama 20)
RIWAYA: Ken Walibora: Kidagaa Kimemwozea. Jibu swali la 2 au la 3
“Wachache hawa hawaogopi, ashakum si matusi, hata kutema mate au kumwaga
mkojo usoni mwa haki, usawa na uhuru uliopiganiwa na kumwagiwa damu…”
a) Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
b) Tambua mbinu ya lugha iliyotumika katika dondoo hili. (alama 2)
c) Huku ukitoa mifano fafanua jinsi mwandishi alivyoshughulikia suala la ukiukaji
wa haki katika riwaya ya Kidagaa Kimemwozea. (alama 14)
20 marks
Eleza jinsi mwandishi wa Kidagaa Kimemwozea ameshughulikia mbinu ya kisengere
nyuma katika kuwasilisha ujumbe wake.
20 marks
SEHEMU YA C (Alama 20)
TAMTHLIA Timothy Arege: Mstahiki Meya. Jibu swali la 4 au 5
Mzee akitutunuku heshima ya kutuchagua sisi kuwa siyo tu macho yake bali pia
masikio na sauti yake.
a) Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
b) Tambua tamathali mbili za semi zilizotumika katika dondoo hili. (alama 2)
c) Eleza vile msemaji na mwenzake walivyochangia katika kumpotosha Mzee
anayerejelewa. (alama 14)
20 marks
Ukizingatia tamthlia ya Mstahiki Meya, fafanua jinsi uongozi mbaya unavyoathiri
maisha ya Wanacheneo.
20 marks
SEHEMU YA D (Alama 20)
HADITHI FUPI. Ken Walibora na Said A. Mohamed: Damu Nyeusi. Jibu swali la 6 au 7
Huoni mwenyewe, wala hupimi? Fikira zako ziko wapi na zangu ziko wapi?
a) Eleza muktadha wa dondoo hili. (alama 4)
b) Msemaji wa kauli hii alikuwa ametambua udhaifu gani katika maisha ya
mzungumziwa? (alama 3)
c) Ni chngamoto gani msemaji alikumbana nazo katika kuimarisha uhusiano wake na
msemaji? (alama 3)
d) Eleza vile msemaji alivyotofautiana kifikira na msemewa. (alama 10)
20 marks
Maudhui ya ubabedume yamejitokeza katika diwani ya Damu Nyeusi na Hadithi Nyingine.
Jadili suala hili kwa kurejerea hadithi zifuatazo:
i) Maeko
ii) Samaki wa Nchi za Joto.
iii) Kikaza
iv) Mke Wangu.
20 marks
SEHEMU YA E (Alama 20)
FASIHI SIMULIZI.
(a) Huku ukitoa mifano, eleza tofauti kati ya istilahi zifuatazo za Fasihi Simulizi:
(i) Ngano za mtanziko na hekaya. (alama 2)
(ii) Ngano za usuli na visasili. (alama 2)
(b) (i) Ngomezi ni nini? (alama 2)
(ii) Eleza dhima ya ngomezi. (alama 5)
(iii) Fafanua sifa nne za ngomezi. (alama 4)
(iv) Eleza udhaifu wa ngomezi katika jamii zinazoitumia. (alama 5)
20 marks