KNEC KCSE Past Papers 2019 Kiswahili Karatasi ya 1 (102/1)
Kenya Certificate of Secondary Education Kiswahili Karatasi ya 1 – Insha
1. Lazima
Wewe ni Mkuu wa Elimu katika kaunti ndogo ya Tuangaze. Andika hotuba utakayowatolea Maafisa wa Elimu na Walimu Wakuu kuhusu umuhimu wa kustawisha vyuo vinavyotoa mafunzo ya kiufundi katika eneo lao.
2. “Usalama wa mwanafunzi unamtegemea yeye.” Jadili.
3. Andika insha itakayodhihirisha maana ya methali ifuatayo:
Mla nawe hafi nawe ila mzaliwa nawe.
4. Andika kisa kinachoanza kwa maneno yafuatayo:
Nilimtazama kwa muds.
Moyo wangu ulinituma kumuuliza kilichomfanya kuishi katika mazingira ya kudhalilisha kama hayo.
Kiswahili Karatasi 1 (102/1)
Majibu
1. Hii ni hotuba. Vipengele viwili vikuu vya hotuba vizingatiwe:
(a) Maudhui
(b) Muundo
I. Muundo
Sura ya hotuba idhihirike:
a) Anwani
b) Mwanzo
(i) Salamu: mtahiniwa atambue waliohudhuria kwa vyeo, kuanzia kwa aliye na cheo cha juu zaidi.
(ii) Katika aya hii mtahiniwa abainishe kiini cha hotuba: kuzungumzia umuhimun wa vyuo vinavyotoa mafunzo ya kiufundi.
c) Hapa ndipo mtahiniwa atakapojadili hoja kuhusu umuhimu wa vyuo vya kiufundi. Kila hoja ijadiliwe kwa kina kwa mtindo ufaao. Mtahiniwa azungumze moja kwa moja na hadhira/ atumie nafsi ya kwanza.
d) Hitimisho
(i) Mtahiniwa ahitimishe hotuba kwa kubainisha msimamo wake kuhusu umuhimu wa vyuo vinavyotoa mafunzo ya kiufundi.
(ii) Aya hii ibainishe fomyula maalumu ya kufunga hotuba, hususan awashukuru waliohudhuria.
I. Maudhui
Mtahiniwa abainishe umuhimu wa kustawisha vyuo vinavyotoa mafunzo ya kiufundi. Baadhi ya hoja ni:
(i) Kuwapa wanafunzi ambao hawakupata nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza/vyuo vinavyotoa Stashahada/ vyuo vikuu fursa ya kujiendeleza kielimu/kitaaluma.
(ii) Kukabiliana na uhaba wa nafasi za kazi — wanaohitimu wanaweza kujiajiri na kuwaajiri wengine.
(iii) Kuziba pengo la ukosefu wa mafundi, kama vile waashi, mafundi wa umeme na wa mabomba ya maji.
(iv) Kukabiliana na mawazo/mtazamo hasi kuwa wanaofanikiwa ni wale tu wanaopata elimu ya kiakademia.
(v) Kupunguza visa vya uhalifu kwa kuwahusisha vijana katika masomo badala ya kuwaacha kukata tamaa na kujiingiza katika uhalifu.
(vi) Kupunguza uhamiaji mijini kufuatia mafunzo haya/ kitaaluma.
(vii) Kukuza vipawa vya vijana ajira isiyohitaji mafunzo
(viii) Kuimarisha ubunifu. Vijana wanaweza kuanza kuwa wajasiriamali mapema na kubuni nafasi za kazi kwa wenzao.
(ix) Kuwapunguzia wakazi gharama kwa kuunda bidhaa za bei nafuu, badala ya kwa mfano, kuwalazimu kununua bidhaa zilizoagizwa.
(x) Kupunguza msongamano katika vyuo vya kiufundi vya kitaifa.
(xı) Kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na ya kijamii katika nchi/ kukabiliana na tatizo la umaskini.
(xii) Kubuni nafasi za ajira kwa wataalamu na wafanyakazi: walimu/ wakufunzi kuajiriwa katika vyuo hivi.
(xiii) Wanaohitimu vyuoni kutoa huduma bora kwa malipo nafuu.
2. Hii ni insha inayohusu suala ibuka. Ni insha ya kimjadala. Insha hii inamhitaji mtahiniwa kuwa amesoma kwa mapana ili kumudu kuikuza mada ipasavyo.
Yafuatayo yazingatiwe:
(i) Mtahiniwa aonyeshe umuhimu wa mwanafunzi katika kujihakikishia usalama wake.
(ii) Anaweza kuonyesha mambo ambayo anaweza/anapaswa kufanya iii kuhakikisha yu salama au yale ambayo anapaswa kuepuka iii awe salama.Mtahiniwa anaweza kuchukua mwelekeo huu kuanzia mwanzo hadi mwisho wa utungo.
(iii) Mtahiniwa anaweza pia kujadili pande zote mbili, akaonyesha umuhimu wa mwanafunzi katika kujihakikishia usalama, na vile vile nafasi ya wengine kama vile uongozi wa shule katika kuimarisha usalama. Hata hivyo, msimamo wake sharti ujitokeze mwishoni mwa utungo.
(iv) Kuna baadhi ambao watachukua mtazamo ya kwamba usalama wao hauwategemei, kuna vizingiti, pengine kutokana na ulemavu, au hadhi yao duni kiuchumi na kijamii inayotinga hatua za kujihakikishia usalama. Mtahiniwa wa aina hii, sharti atoe ithibati kuonyesha kwamba usalama wao unawategemea wengine; hawezi kujihakikishia usalama.
Baadhi ya hoja zinazoweza kujadiliwa ni:-
(i) Kuhakikisha anaishi katika mazingira salama yaliyozingirwa. Kwa mfano, kufunga mlango anapolala.
(ii) Kuepuka michezo/shughuli zinazoweza kusababisha kuumia.
(iii) Kutokula chakula kinachoweza kudhuru afya.
(iv) Kujinadhifisha iii kujikinga dhidi ya magonjwa.
(v) Kunadhifisha mazingira ili kujikinga na vifaa/wanyama/wadudu waharibifu.
(vi) Kujiepusha na utekwaji nyara kwa kutotembea usiku/kutoandamana na asiowajua (vii) Kujifunza kutumia vifaa kama vile meko ya gesi ili kujikinga dhidi ya moto.
(viii) Kujihakikishia usalama wa kiakili kwa kutosoma/kutosikiliza/kutotazama mambo ambayo yanaweza kusababisha wasiwasi au kukata tamaa.
(ix) Kuhifadhi vitu vyake mahali salama ili visiibiwe.
(x) Kujiepusha na matumizi mabaya ya vileo au dawa ambayo yanaweza kumsababishia fadhaa na hata kufungwa.
(xi) Kuheshimu mali ya wengine ili kuepuka adhabu/kifungo.
(xii) Kuvaa mavazi yanayomsitiri vyema iii kukinga dhidi ya magonjwa yanayosababishwa na hali ya anga, au hata unyanyasaji wa kimapenzi.
(xiii) Kujihakikishia mtazamo kwenye mtandao kwa kusakura matini salama.
(xiv) Kutokubali urafiki kwenye mtandao bila kuwajua wanaomataka urafiki.
(xv) Kutotoa habari za kibinafsi kwenye mitandao ya kijamii.
AU Mtahiniwa anaweza kuonyesha mchango wa wengine. Mifano:
(i) Wazazi pia wanaweza kuimarisha usalama kwa kuhakikisha kuna makao salama.
(ii) Shule kujenga mabweni yenye nafasi za kutorokea patokeapo janga, kama vile la moto.
(iii) Wazazi/shule kuhakikisha kuna vifaa vya kukabiliana na majanga kama vile moto.
(iv) Serikali kuhakikisha kuna wadumishaji usalama shuleni.
(v) WaZaZi kumpa mavazi ya kujisetiri.
(vi) Wazazi kudumisha mahusiano mema baina yao ili kumhakikishia utulivu wa kiakili.
(vii) Taasisi za kielimu kuhakikisha kwamba kuna miundomsingi inayowahakikishia wanafunzi, pamoja na wale wenye mahitaji maalumu usalama
Tanbihi
(i) Atakayeshughuliki a upande wa pili bila kujihusisha atakuwa amepungukiwa kimaudhui.
(ii) Anayeonyesha kwamba usalama haumtegemei yeye sharti aonyeshe udhaifu unaomfanya asiweze kujihakikishia usalama; sharti asadikishe.
3. Kisa kibainishe maana ifuatayo:
Rafiki au mtu ambaye mnasherehekea naye wakati unapokuwa katika hali ya neema au furaha, hukukımbıa wakati wa shida. Hata hivyo mtu uliye na uhusiano wa kinasaba (damu) naye atakaa nawe hata wakati wa matatizo/ wakati unapokupungukiwa.
Hali zifuatazo zinaweza kujitokeza katika hadithi/masimulizi:
(i) Mhusika apandishwe cheo, awe na marafiki wengi, afutwe, marafiki wamkimbie/ wamdharau/wasimsaidie hata kutafuta kazi lakini ndugu amfae angaa kwa chakula na malazi. (ii) Wakati mhusika anakuwa mwenye afya awe na marafiki wengi; apatwe na ugonjwa sugu, wafanyakazi wenzake wamwambae, aila yake ijitolee kumuuguza/ kuchangia matibabu yake.
(iii) Mhusika aoe rnke, mke ampende wakati anapokuwa na mali. mke amdharau na kumwacha; abaki kuwategemea ndugu.Anapoishiwa na mali
1. Kwa vyovyote vile pande zote za methali sharti zijitokeze.
(i) Mla nawe – Rafiki anayesherehekea nawe.
Mhusika asawiriwe akishirikiana na rafiki kwa mengi wakati wa furaha.
(ii) Hafi nawe
Hali ya rafiki kutovumiliana/kutoandamana na mhusika wakati wa matatizo/kupungukiwa.
(iii) Ila mzaliwa nawe – Hali ya kinyume ijitokeze ambapo ndugu anamsaidia mhusika wakati wa matatizo/kupungukiwa.
11. Mtahiniwa akizingatia upande mmoja atakuwa amepungukiwa kimaudhui.
4. Mtahiniwa atunge kisa kinachoanza kwa kauli aliyopewa. Kisa kioane na hali inayofumbatwa na kauli hii. Toni na mazaji ya masimulizi ziafikiane na toni na mazaji ya kauli hii. Hali zifuatazo zinaweza kubainika katika usimulizi:
(i) Mhusika anayetazamwa na msimulizi yumo katika mahali/mazingira duni; pengine katika jalala/jaa akiokota chakula kilichotupwa.Pengine msimulizi alimjua mhusika hapo awali.
(ii) Msimulizi amekutana na mhusika mahali penye aibu, pengine anafanya kazi kwenya baa; pengine hata danguroni.
(iii) Pengine mhusika ana elimu ya juu, naye anafanya kazi kama vile ya uhamali sokoni naye msimulizi aneshawishika kumuuliza.
(iv) Mhusika /mtoto anaweza kuwa amelelewa katika mazingira ya kitajiri akatorokea mjini na kuishi maisha ya kudhalilisha kama vile kuvuta gundi. Anayemtazama anashangaa.
(v) Mtu mwenye nafasi/cheo anapatikana katika mazingira ya kuaibisha kama vile danguroni, au mkahawa wa hadhi ya chini.
(vi) Msimulizi huenda amempata mhusika katika jela, akashangaa kilichompelekea kuishi humo.
(vii) Pengine awali mhusika alikuwa ameolewa, naye msimulizi anampata katika mazingira ya kudhalilisha. Pengine ndoa imevunjika, msimulizi anashangaa.
Si lazima msimulizi amuulize mhusika swali anaweza kubadilisha mkondo wa masimulizi. Baada ya kauli hii, msimulizi anaweza, ama kuendeleza kisa, akasimulia yaliyotokea baada ya fıkira hii, au akaturudisha uyuma (mbinu rejeshi) kutuhadithia yaliyosababisha hali hii/ yaliyofanyika hata wote wawili wakawa hapa.
(iii) Kisa kinaweza kuendelezwa kwa nafsi ya kwanza, ya tatu au mchanganyiko wa nafsi.
Thank you so much