KNEC KCSE Kiswahili Paper 2 Question Paper / 2015 KCSE Kericho West Joint Examination
2015 KCSE Kericho West Joint Examination
Kiswahili Paper 2
1. UFAHAMU (Alama 15)
Soma taarifa hii kisha ujibu maswali yanayofuata.
Alipokuwa akiukemea utamaduni na dhana za kikabila katika nyimbo zake, marehemu Bob Marley aliufananisha ubepari na “wanyama wala watu.” Katika wimbo “Babylon System” (yaani mfumo wa kibepari), Marley alisema kuwa utamaduni huo ndiyo mzawa wa matatizo yote ya kiutawala ambayo yalikuwa yakiyakumba mataifa ya Weusi katika karne ya 20, wakati nchi zao zilikuwa zikitawaliwa na nchi za mataifa ya Ulaya.
Kwa mantiki hiyo, pengine Marley alikuwa na maono kuwa Afrika haingejikomboa kutoka kwa utumwa wa Kizungu, ikiwa ingeendelea kuziabudu na kuzishadidia tamaduni za Kimagharibi.
Utabiri huo nauoanisha na yanayoendelea nchini, ambapo serikali ya Jubilee imeonekana kushindwa kabisa kuikabili saratani ya ufisadi, ambayo inahatarisha kuliamgamiza taifa hili lenye uchumi dhalili.
Donda hili linazidi kuyatandaza mabawa yake kutoka, tisho kuu likiwa ni uvamizi wa taasisi “takatifu” ambazo tunazitegemea kulikabili donda hilo.
Ni nani tutategemea kukabiliana na rushwa ikiwa taasisi kama Bunge, Tume ya Maadili na Kukabiliana na Ufisadi (EACC) kati ya zingine muhimu zimepakwa tope na saratani hiyo?
Kimsingi yote tunayopitia ni matunda ya uasi wa tamaduni za Kiafrika na uegemezi wa mifumo ya Kizungu kama mihimili ya jamii na nchi zetu.
Ndoto za watetezi wa Uafrika na nafasi ya Weusi kama marehemu Malcom X na Martin Luther King, zilikuwa ni kuona kuwa wameungana kabisa kukabiliana na matatizo yaliyowakabili bila kuzingatia mazingara waliyokuwepo.
Pindi tu baada ya mataifa mengi ya Kiafrika kujinyakulia uhuru wao katika miaka ya hamsini na sitini, viongozi wakuu walioziongoza nchi hizo kama Kwame Nkrumah, Jomo Kenyatta, Mwalimu Julius Kibarage Nyerere kati ya wengine walianza harakati za kuliunganisha bara hili na kubuni Muungano wa Nchi za Kiafrika (USA) japo ndoto hiyo haikufikia.
Kwa msingi huo, mhimili mkuu wa kiutawala ungekuwa ni mfumo wa kisochalisti, ambao ungekuwa nguzo kuu ya kuyaunganisha mataifa hayo.
Hata hivyo, migawanyiko mikubwa ilianza kushuhudiwa, huku baadhi ya mataifa yakianza kukabiliwa na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe, huo ndio ulikuwa mwanzo wa kutaasisika kwa maovu yote tunayoshuhudia sasa-ufisadi na tamaa ya kuogofya kutoka kwa viongozi wetu.
Maswali
a. Ipe taarifa hii anwani mwafaka. (alama 1)
b. Onyesha mambo mawili makuu ambayo msanii aliyapinga. (alama 2)
c. Kwa nini ubepari umelinganishwa na ‘wanyama wala watu’.? (alama 2)
d. Kwa mujibu wa taarifa eleza sifa za Bob Marley. (alama 2)
e. Swala linalozugumziwa limerejelewa kama ‘Donda’.
i) Eleza mbinu ya lugha iliyotumika.. (alama 2)
ii) Ni kweli kuwa donda hili laelekea kuwa gumu. Thibitisha. (alama 2)
f. Tatizo hili la ‘donda’ ni kama kujipalia makaa. Fafanua. (alama 2)
g. Eleza maana ya maneno yafuatayo kwa mujibu wa taarifa. (alama 2)
i) Mhimili
ii) Taasisi
15 marks
2. UFUPISHO (Alama 15)
Soma taarifa ifuatayo kisha ujibu maswali.
Sisi vijana wa Kenya inatupasa kufanya kazi kwa bidii na kwa dhati ya mioyo yetu ili tuweze kupata ufanisi na uwezekano wa kuinua nchi yetu change katika kiwango cha juu. Tukumbuke, “Ajizi ni nyumba ya njaa.” Kwa hivyo basi haifai kulaza damu ikiwa matatizo nchini mwetu yametuzonga. Lazima tufanye kazi kwa busara, adabu njema na jitihada kwa moyo mmoja. Sharti tutilie maanani zaidi elimu ya vijana na watu wazima, kilimo, uchumi na amani katika nchi yetu. Tunahitaji taifa lenye watu walioelimika, kwani bila elimu itakuwa vigumu sana kuweza kutekeleza mipango mbalimbali ya mazao mashambani kwani kila kukicha idadi ya watu inaongezeka. Ni sharti tuweze kujitosheleza kwa chakula. Zaidi ya hayo, lazima tujishughulishe na biashara ambapo kwa sasa ni Wakenya wachache sana ambao wanatambua umuhimu wa biashara. Wengi ni wale wenye mawazo ya kwamba lazima kila mmoja aajiriwe maishani. Yatupasa kujitahidi kuleta uchumi katika mikono ya wananchi wa Kenya badala ya kuwaachia wengine ambao hawahusiki.
Mafunzo tunayopata majumbani, shuleni na hata katika jamii, lazima yatuwezeshe kutambua mbinu za kupitia. Tunahitaji elimu tambuzi ambayo itamfanya mwanakenya kujua wajibu wake katika jamii. Tumesinywa na elimu pumbao inayotupumbaza na kutufanya tusione mbele. Sisi vijana tukiwa viongozi wa siku zijazo tutambue kwamba ‘Utengano ni uvundo’. Lugha ya taifa ndiyo chombo cha pekee ambacho kinatuunganisha na kuweza kutuwasilishia mapendekezo, mawaidha na hisia zetu. Kukosa ndiko binadamu. Wakati tunapokosea lazima tukubali kuwa tumekosa na kufanya masahihisho mara moja kwani, “Usipoziba ufa, utajenga ukuta.” Tusikasirike kwa sababu tumesahihishwa makosa yetu na wenzetu. Lazima tujitoe mhanga na kupigania nchi yetu tukiwa
wazalendo halisi.
Sisi tukiwa vjana sharti tujishughulishe na kuyaangalia matatizo ya nchi, pia kutafuta njia za kutatua matatizo hayo. Siku zote tutekeleze nidhamu. Ni jambo la kusikitisha kwamba sisi vijana twashutumiwa mara kwa mara kwa kutokuwa na nidhamu shuleni na majumbani mwetu. Ili watu waweze kuishi maisha bora na kuwa na maendeleo, amani na upendo, lazima tuwe na bidii, ushirikiano mwema na kuchagua viongozi wenye mioyo ya maendeleo. Tukiwa viongozi ambao hawajishughulishi na maendeleo basi tutabaki nyuma kama mkia siku zote.
Bahati mbaya ni kwamba wananchi wengi siku hizi huchagua viongozi wao kwa kufuata ukoo ama kwa utajiri wake. Kwa hivyo basi ni vyema kuwachagua viongozi kutokana na ufanisi wanaoweza kuleta bali si kwa kutegemea utajiri au ukoo.
Maswali
a) Katika aya ya kwanza mwandishi anawahimiza vijana kufanya nini ili kuchangia katika maendeleo? (maneno 45- 50) (alama 7)
b) Fupisha aya mbili za mwisho kwa maneno 50 – 60. (alama 8)
15 marks
3. MATUMIZI YA LUGHA (Alama 40)
Taja sifa mbili za kutambua irabu.
2 marks
Tunga sentensi kwa kutumia kitenzi cha katika kauli ya kutendeka.
2 marks
Tunga sentensi kwa kutumia nomino ifuatayo katika hali ya wingi.
Uyoga
2 marks
Andika katika usemi halisi.
Mama alinifokea nitoke hapo mara moja.
3 marks
Unda nomino ya dhahania kutokana na kitenzi kifuatacho na uitungie sentensi sahihi.
Batili
2 marks
Changanua sentensi ifuatayo kwa kielelezo cha vishale.
Mzigo ubebwao una uzani mkubwa.
4 marks
Akifisha:
umoja wa mataifa barani afrika akaanza mwinyi utaimarishwa na viongozi wa nchi hizi ili tuendeleze maendeleo kupitia utandawazi akamaliza
3 marks
Andika sentensi ifuatayo katika ukubwa wingi.
Mkono wa yule mwizi ulikatwa kwa upanga wenye makali.
3 marks
i) Eleza maana ya shamirisho. (alama 2)
ii) Bainisha shamirisho katika sentensi hii. (alama 2)
Buzi lililochinjiwa wageni lilipaswa kuuzwa kesho asubuhi.
4 marks
Eleza matumizi matatu tofauti ya kiambishi -ka-
3 marks
Ainisha vitenzi katika sentensi hii.
Ukweli ulio na uchungu haupendwi.
3 marks
Ainisha viambishi katika sentensi hii:
Kilichofungishwa
3 marks
Andika maana mbili ya neno : Karo
2 marks
Kanusha:
Wao wakimbiapo huwa wameona hatari.
2 marks
Tunga sentensi kwa kutumia kinyume cha kitenzi angika.
2 marks
Amrisha katika wingi.
Amka
1 marks
4.ISIMU JAMII (Alama 10)
a) Eleza maana ya mawasiliano. (alama 2)
b) Taja njia tatu ambazo kwazo mwanadamu huwasiliana. (alama 3)
c) Eleza sababu zinazochangia kuwepo kwa uwingi lugha. (alama 5)
2 marks