Sudan kusini
udan Kusini (jina rasmi: Jamhuri ya Sudan Kusini, kwa Kiingereza Republic of South Sudan) ni nchi huru iliyojitenga rasmi na Sudan tarehe 9 Julai 2011, ikiwa ni ya 54 katika bara la Afrika na ya 193 duniani.
Hatua hiyo ilitokana na kwamba mwezi wa Januari 2011 wakazi wa Sudan Kusini walipiga kura juu ya swali la kujitenga na Sudan wakaamua karibu kwa kauli moja (98.83%) kuwa nchi huru.
Tofauti kubwa kati ya pande hizo ilikuwa kwamba katika Sudan yenyewe idadi kubwa ya watu wamekuwa Waislamu na utamaduni wao una mchaganyiko wa tabia za Kiarabu na Kiafrika pamoja na usambazaji mkubwa wa lugha ya Kiarabu. Kumbe kusini kuna Waislamu wachache, wengi ni wafuasi wa dini za jadi au ni Wakristo. Kiuchumi na kielimu kusini wako nyuma sana kulingana na kaskazini.
Nchi ina muundo wa shirikisho.
Tangu upatikane uhuru, nchi imeendelea kuvurugwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe na kwa sasa inashika nafasi ya kwanza katika orodha ya nchi dhaifu.
Mji mkuu ni Juba, wenye wakazi 1.118.233.
Imepakana na Sudan kaskazini, Ethiopia mashariki, Kenya, Uganda, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kusini, na Jamhuri ya Afrika ya Kati upande wa magharibi.
Inakadiriwa kwamba Sudan Kusini ina wakazi 12,340,000 (2015), lakini kutokana na ukosefu wa sensa kwa miongo kadhaa, makisio haya yaweza kuwa si sahihi.
Uchumi unategemea kilimo vijijini na cha kujikimu, lakini mwanzoni mwa mwaka 2005, uchumi alianza mpito wa kutoka vijijini na mijini katika Sudan Kusini kumeonekana maendeleo kupindukia.
Mnamo Machi 2016 nchi imefaulu kujiunga na Jumuia ya Afrika Mashariki kama mwanachama wa sita.